Katika kusherehekea Siku ya Kiswahili, tunaangazia Balozi Pharence Oluoch Nduko, mtangazaji wa mpira wa miguu, maisha yake yamebadilishwa na mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom. Mashindano ambayo imefanyika kwa misimu ya nne sasa. Chapa Dimba inawapa vijana fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kujenga maisha yao kupitia michezo.
Alianza kama shabiki wa mpira wa miguu na ripota wa mchezo wa mpira mashinani Radio Citizen baadaye alipata nafasi ya kuwa mtangazaji wa Chapa Dimba. “Nafasi yangu kama mtangazaji wa Chapa Dimba imeathiri sana ustadi wangu na shukrani yangu kwa lugha ya Kiswahili,” anasema Balozi. “Kiswahili kimenisaidia sana kuwasiliana kwa urahisi na kueleweka na hadhira. Lugha hii imekuwa muhimu katika kuleta uelewa na mshikamano kati ya wachezaji na mashabiki.”
Balozi anakumbuka jinsi alivyotoka Nairobi kuelekea Kakamega kutafuta nafasi ya kutangaza mashindano ya Chapa Dimba. Ingawa hakumjua mtu yeyote huko, alipata nafasi ya kuzungumzia Chapa Dimba na kusalimia mashabiki, ambapo sauti yake ilikubalika sana. Safari hii ilimpa nafasi isiyotarajiwa ya kuonesha uwezo wake mkubwa wa matangazo, na hivyo kujitengenezea jina katika uwanja wa matangazo ya mpira.
Katika kazi yake ya utangazaji na uchanganuzi wa kabumbu, Balozi ametumia Kiswahili kama chombo muhimu cha mawasiliano. “Kiswahili ni lugha ambayo kila mtu anaelewa, inapendwa na wengi, Inasaidia kufikisha ujumbe kwa urahisi na inaunganisha watu kwa njia ya kipekee,” anelezea.
Kushiriki katika Chapa Dimba kumeathiri maisha ya Balozi binafsi na kitaaluma kwa njia nyingi. Chapa Dimba imeimarisha ujuzi wake wa mawasiliano, kumtuza fursa nyingi za kitaaluma na kujenga urafiki na uhusiano mzuri na watu mbalimbali. “Siku ya Kiswahili ni muhimu sana kwani inatukumbusha asili yetu na umuhimu wa lugha katika kuimarisha utamaduni na mshikamano.” Balozi anasema.
Matumizi ya Kiswahili katika Chapa Dimba yameimarisha hisia za jamii na utambulisho miongoni mwa washiriki na mashabiki. Mwaka huu, maudhui ya Siku ya Kiswahili ni “Elimu ya Kiswahili na Utamaduni wa Amani.” Umuhimu wa elimu katika kuendeleza lugha ya Kiswahili ni kudumisha utamaduni na itawezesha jamii kujivunia na kuienzi lugha yao.
Safaricom, kama kampuni inajivunia utamaduni na lugha ya Kiswahili. Safaricom imekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili. Bidhaa mbalimbali za Safaricom zinapatikana kwa lugha ya Kiswahili, ikiwemo huduma za simu za mkononi, na vifurushi vya data. Lugha hii ni muhimu sana katika mawasiliano ya kila siku kati ya wateja na wahudumu wa kampuni.
Katika kusherehekea Siku ya Kiswahili, tunatambua na kuthamini umuhimu wa lugha hii katika kuleta mshikamano na utambulisho katika jamii yetu. Kazi ya Balozi Pharence na mchango wake katika Chapa Dimba ni mfano mzuri wa jinsi Kiswahili kinavyoweza kubadilisha maisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.